Hosea 2:1-13

1 a“Waambie ndugu zako, ‘Watu wangu,’ na pia waambie dada zako, ‘Wapendwa wangu.’

Israeli Aadhibiwa Na Kurudishwa

2 b“Mkemeeni mama yenu, mkemeeni,
kwa maana yeye si mke wangu,
nami si mume wake.
Aondoe sura ya uzinzi katika uso wake
na uzinzi kati ya matiti yake.
3 cKama sivyo nitamvua nguo zake awe uchi
na kumwacha uchi kama siku ile aliyozaliwa.
Nitamfanya kama jangwa,
nitamgeuza awe nchi ya kiu,
nami nitamuua kwa kiu.
4 dSitaonyesha upendo wangu kwa watoto wake,
kwa sababu ni watoto wa uzinzi.
5 eMama yao amekosa uaminifu
na amewachukua mimba katika aibu.
Gomeri alisema, ‘Nitawaendea wapenzi wangu,
ambao hunipa chakula changu
na maji yangu,
sufu yangu na kitani yangu, mafuta yangu
na kinywaji changu.’
6 fKwa hiyo mimi Mungu nitaizuia njia yake
kwa vichaka vya miiba,
nitamjengea ukuta ili kwamba
asiweze kutoka.
7 gGomeri atawafuatia wapenzi wake lakini hatawapata;
atawatafuta lakini hatawapata.
Kisha atasema,
‘Nitarudi kwa mume wangu kama kwanza,
kwa maana nilikuwa na hali njema zaidi
kuliko sasa.’
8 hGomeri hajakubali kuwa mimi ndiye
niliyempa nafaka, divai mpya na mafuta,
niliyemwongezea fedha na dhahabu waliyoitumia
kwa kumtumikia Baali.

9 i“Kwa hiyo nitachukua nafaka yangu wakati itakapokomaa
na divai yangu mpya wakati itakapokuwa tayari.
Nitamnyangʼanya sufu yangu na kitani yangu
iliyokusudiwa kufunika uchi wake.
10 jBasi sasa nitaufunua ufisadi wake
mbele ya wapenzi wake;
hakuna yeyote atakayemtoa
mikononi mwangu.
11 kNitakomesha furaha na macheko yake yote:
sikukuu zake za mwaka,
sikukuu za Miandamo ya Mwezi,
siku zake za Sabato,
sikukuu zake zote zilizoamriwa.
12 lNitaiharibu mizabibu yake na mitini yake,
ambayo alisema yalikuwa malipo yake
kutoka kwa wapenzi wake;
nitaifanya kuwa kichaka,
nao wanyama pori wataila.
13 mNitamwadhibu kwa ajili ya siku
alizowafukizia uvumba Mabaali;
alipojipamba kwa pete
na kwa vito vya thamani,
na kuwaendea wapenzi wake,
lakini mimi alinisahau,”
asema Bwana.
Copyright information for SwhNEN